Hermy B wa B-Hits Aamua Kutoa ya Moyoni Kuhusu Yaliyotokea B-Hits Mpaka Wasanii Kukimbia
Producer na CEO wa Bhitz Music Group, Hermy B ameandika barua ya wazi
akielezea yaliyowahi kutokea Bhitz, uamuzi na mpango wao mpya.
Hivi ndivyo alivyoandika Hermy B:
Nikiwa kama CEO wa B’hitz Music Group na Producer ambaye napigana kama
producers wengine kuusogeza muziki wa Tanzania katika level fulani,
sikupendezwa kabisa na jinsi ambavyo baadhi ya watu walivyoizungumzia
B’hitz na jinsi ambavyo baadhi yao wanaichukulia..
Kutokana na yote yaliyozungumzwa na baadhi ya wasanii ambao
tulitofautiana nao kikazi, wengi wametuchukulia kama sisi ni wagomvi na
wanyonyaji.
Lakini ukweli ni kwamba hakuna msanii ambaye alishatengeneza faida ya
kifedha kwa B’hitz na wasanii hao walikuwa wakifanya kazi bila malipo
yoyote na hata walipokuwa wakifanya shows tulikuwa tukiwaachia pesa kwa
kuwa tulifahamu bado muda mzuri wa mavuno kulingana na ubinadamu,
makubaliano na malengo, hivyo hakuna ukweli kuhusu hilo.
Hata hivyo, tumeyachulia yote yaliyotokea kama sehemu ya changamoto
katika kazi hii ngumu ya muziki Tanzania ambayo kwa kiasi kikubwa
watayarishaji wa muziki hawafaidiki nayo kama ilivyo kwa wasanii ambao
wamejaliwa kuwa na ushawishi mkubwa zaidi kwa jamii na kuaminika mara
moja kwa kile wanachokisema kuhusu sisi pale tunapotofautiana.
Kwa bahati mbaya, mipango tunayopanga nao tunapokuwa studio ama
makubalinao mengi tunayoweka kwa ajili ya kazi zao hayajulikani kwa
umma, na pindi wanapoyakiuka na kusababisha sisi kurudi nyuma
tunaonekana wakosaji na wacheleweshaji wa maendeleo yao.
Naamini wasanii na sisi ndio tunaofahamu ukweli ni upi kati ya yote
yaliyosemwa kupitia media kwa kuwa tunafahamu wapi tumetoka pamoja,
tulikubaliana nini na wapi tulipotofautiana na yupi kati yetu aliacha
reli ya makubaliano.
It’s a new chapter, na tunawatakia kila la kheri wasanii wote waliopita
B’hitz na milango iko wazi kwa msanii yeyote wa Tanzania. Lengo letu ni
kuendelea kuisupport jamii yenye vipaji kwa maendeleo ya taifa hili
linalosifika kwa vipaji.
Nafasi ipo kwa wasanii wote walioondoka na kuacha kazi zao B’hitz, najua
wanajua ni muziki mzuri na tusingependa kuona ukipotea au tukiutoa kwa
kufuata ratiba tulizowekeana awali wakati ambapo wao hawapo.
Wasanii wanaweza kufuata nyimbo hizo na tutakuwa na makubaliano fair ili
maisha ya muziki tulioutengeneza kwa ubunifu wa hali ya juu yaendelee
na watanzania wafaidike kwa kuusikiliza.
Tunaamini uwezo wa Bhitz kuinua vipaji ambavyo havina majina makubwa na
kuvifanya ‘brand’ ni baraka ambayo inabidi iendelee kwa vipaji vingine
ambavyo bado havijajulikana na vina uwezo mkubwa.
Hivyo, tunapenda kuuarifu umma wa watanzania kuwa Bhitz imefungua
ukurasa mpya na hatuendelei kuyashikilia tena matatizo yaliyokuwepo na
wasanii hao.
Tunafurahi pia kuona muziki tuliotengeneza nao wakati tukiwa pamoja
unawapa nafasi kubwa na kuwasogeza katika ngazi nyingine, tunaamini
wanatoa shukurani zao kwa Mungu na zinatufikia kwa kiasi tunachostahili.
Tunaamini tutafika mbali na tumekomazwa zaidi na yaliyojiri kwa kuwa tumejifunza pia, yale ni mapito.
Music shall continue to live and flow in our bloods, we shall support
Tanzanian music and musicians with all our hearts, We shall not give up
because we are a part of this beautiful musical community in Tanzania.
Katika hatua nyingine, ningependa kuungana na producers wengine kuyatoa
ya moyoni pia kuhusu kilio cha watayarishaji wa muziki Tanzania ambacho
kimeendelea kuonekana kama kilio cha samaki. Huenda ni kutokana na
idadi yetu ndogo kulinganisha na wasanii hivyo kilio chetu hakina sauti
kubwa au ni mfumo mzima wa Industry ya Tanzania ulivyo mbaya na
umezoeleka!
Producers wengi Tanzania tumekuwa tukitumiwa na baadhi ya wasanii kama
daraja la mafanikio yao na kisha kutupaka matope au kuuambia umma kuwa
sisi ndio tumewakosea sana na tunawanyonya.
Laiti kama wasanii hao wangekuwa wanaeleza angalau mazuri wanayofanyiwa
na producers. Kwa bahati mbaya sifa wanazotumwagia tunapokuwa studio
tunafanya kazi huishia studio na umma husikia tu wimbo mzuri ukiwa
umetoka. Sifa zetu tunazopewa zimekuwa ‘perishable’ ingawa kazi
tunayofanya huishi miaka yote na hutumiwa na msanii husika.
*Kwa mazoea ya soko la Tanzania, producers wengi huwa na moyo wa mshumaa
na hata kuwatengenezea wasanii wetu midundo au nyimbo bure. Lakini wapo
pia ambao huwalipisha wasanii kiasi cha fedha ambacho kwa uhalisia wa
kazi na matunda ya kazi hii sio halali/sio fair bali ni bei
zilizozoeleka tu.
Kwa uhalali wa ‘intellectual works’ wahusika wakuu huvuna matunda pamoja
kwa kugawana asilimia kila wakati ambapo kazi hiyo itakapokuwa
ikiingiza pesa. Lakini kwa Tanzania ni kama producer humuuzia haki
miliki ya kazi nzima msanii kwa shilingi kadhaa au hata bure na kisha
msanii kuingiza mamilioni kwa miaka mingi kwa kuuza au ku-perform kazi
ile.
Hata kama ni kweli tasnia ya sanaa ya muziki kwa Tanzania bado
inawanyonya wadau kwa ujumla, kati ya hao wanaonyonywa tumkumbuke
producer ambaye yeye ananyonywa hadi damu ya mwisho na kisha kuchafuliwa
pale anaponyoosha mikono yote kutaka mambo yaende sawa.
Hebu fikiria, kama kweli mgao wa matunda ya kazi yangekuwa sawa kwa
asilimia kadhaa kwa kila kazi ambayo producer amefanya, producer kama
P-Funk Majani angekuwa na maendeleo kiasi gani kutoka kwenye muziki
pekee? Sisemi moja kwa moja kama aliofanya nao kazi walimnyonya,
inawezekana alinyonywa na mfumo ulivyo.
Lakini ni wasanii wangapi tumeshawasikia wakitaja mafanikio makubwa
waliyoyapata kwenye muziki kwa hits chache au hata hit moja tu. Je,
umeshajiuliza producer wake alipata nini?
Je, ni producers wangapi ambao wametengeneza hits kibao zilizowapeleka
wasanii mbali sana lakini wao wamebaki na hali ngumu kimaisha huku
wakiendelea kunyonga midundo na kuambulia sifa za studio?
Uzalendo na moyo wa pekee tuliopewa usiokata tamaa kwenye muziki huu
ndicho kitu pekee kinachotufanya tuendelee kuwekeza kwenye huu muziki na
kuinua vipaji vipya na kuendeleza vilivyopo kwa imani kuwa ipo siku
tutavuna matunda kwa kiasi tunachostahili.
Lakini kwa nini hiyo siku isiwe LEO? Itawezekana kama tutaungana na kuungwa mkono na wapenzi wa muziki mzuri.
Nisingependa kutaja majina ya producers wanaowalilia wasanii lakini
karibia producers wote wamekuwa wakifanya hivyo na vilio vyao hupuuzwa
tofauti na vilio vya wasanii.
Ndugu yangu Master Jay yeye amewahi hata kutoa kauli nzito kuwa wasanii
ni wezi wanatuibia na wanatunyonya sisi maproducer. Alikazia kuwa wizi
huu wa wasanii ni wa aina yake kwa kuwa huiba nguvu ya producers na
kisha kujitangaza kuwa wameingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa kazi ile
ile.
Lamar amewahi kusema wasanii wanapokuja studio huwa wapole na
kukubaliana mengi kuhusu wimbo lakini wimbo unapotoka na wao kufanikiwa
huwasahau kabisa producers walioumiza nao kichwa mwanzoni na hata
‘kuwavimbia’. Lamar pia aliwahi kupata matatizo ya kimkataba na msanii
wa Tanzania ambaye aliamua kusaini tena na Candy n Candy ya Kenya ili
hali akiwa na mkataba mwingine.
Mikataba mingi tunayosaini nao mara nyingi huishia mikononi mwetu pale
wanapovunja japo sheria ya mikataba iko wazi lakini kiuhalisia wasanii
hao ni vigumu kulipa fidia itakayotajwa. Producer huamua kufunika kombe.
Producer Dupy yeye aliweka wazi kuwa sisi producers wa Tanzania ni
masikini kulinganisha na wasanii ambao tunafanya nao kazi na kueleza
ukweli kuwa hata wale wanaoonekana maisha yao ni mazuri ni wale ambao
wanaingiza kipato kupitia shughuli nyingine tofauti na muziki.
Mimi pia ni mmoja kati ya producers ambao wanapata fedha kupitia
shughuli nyingine na fedha hizo naziwekeza tena kwenye muziki kwa imani
kuwa ipo siku mambo yatakuwa mazuri lakini mara nyingi wasanii unaopanga
nao studio wanapopata mabawa (mafanikio) huruka na kueleza mabaya na
sio mazuri mliyofanya nao yaliyowapa hayo mabawa.
Sisemi kuwa sisi hatuwakosei wasanii, tunakoseana kwa kuwa sisi pia ni
binadamu japo sio kwa kiasi hicho wanachosema. Kukoseana katika kazi ni
jambo la kawaida. Kukwaruzana wakati wa ujenzi ni kawaida pia.
Lakini kwa kuwa msanii huyo tayari ni brand, hasara kubwa huwa kwa
producer ambaye inabidi aendelee kufanya kazi nyingine na watu wengine
kwa kuanzisha upya malengo yake huku akiwa amemfaidisha tayari msanii
huyo (Tayari ni brand).
Nyimbo tunazotengeneza nyingi studio tukisubiri msimu wa ‘mvua’ tuupush
zinapobaki huwa hasara kwa producer kwani wao wanaweza kwenda kwa
mwingine na wakazirudia. Je, producer anapata faida gani kwa kazi
aliyoifanya tayari?
*Imefika wakati ambapo producer inabidi aheshimiwe kwa sababu bila yeye
kusingekuwa na wasanii wengi wanaotamba hivi sasa. Hii itaongeza nguvu
pia ya kazi kwa producers wapya nchini.
Producer alipwe vizuri kwa sababu anapolipwa vizuri na yeye ubunifu na
utendaji wake wa kazi unakua kwa kiwango kikubwa. Pia atapata uwezo wa
kununua vitendea kazi bora zaidi vitakavyomsaidia kuingiza muziki wetu
kwenye ushindani wa soko la muziki Afrika na duniani kwa ujumla.
Naamini ipo siku hata haki za producer katika muziki alioutengeneza
Tanzania zitazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuvuna asilimia fulani ya
muziki wake pale unapotumika kwenye miito ya simu, na biashara nyingine.
B’hitz Music Group, inavishukuru vyombo vyote vya habari Tanzania kwa
support yao ikiwa ni pamoja na websites na blogs mbalimbali. Tuendelee
kushirikiana.
This is the time! Sisi tunaendelea na kazi na tunawakaribisha wasanii wote.
Regards.
Hermes B. Joachim
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni