WAKATI msanii wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’,
akiendelea kusaka faraja ya moyo kutokana na kudai kuwa amekuwa
akikabiliana na vitisho, mama yake mzazi ameamua kuondoka nyumbani
kwake akihofia kuuawa.
Nay aliingia kwenye mgogoro na serikali kutokana na wimbo wake wa Wapo
uliosababisha ashikiliwe na jeshi la polisi pamoja na wimbo huo
kufungiwa na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) lakini aliokolewa na
kwa amri ya Rais John Magufuli.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Nay amesema pamoja na tamko la Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, kutoka kwa
rais, kuruhusu wimbo wake uchezwe kote, ameendelea kuwa na vitisho kila
kukicha kutoka kwa watu asiowafamu.
“Ninaishi kwa mashaka makubwa, tangu nilipoachia wimbo huu, maana
kumekuwa na mfululizo wa kupigiwa simu na meseji za watu wakinitishia
maisha jambo ambalo limepelekea hadi mama yangu kuamua kuhama nyumbani
kwangu na kurudi kwake.
“Kabla sijatoa wimbo huu nilikuwa naishi na mama nyumbani kwangu, lakini
ameamua kuondoka kufuatia kutishiwa maisha kila kukicha, lakini baya
zaidi vitisho hivyo vimenifanya mimi na mama kupishana mawazo ambapo
ameniambia niachane na wimbo huo, tena ikiwezekana niachane na muziki
ili nifanye biashara zingine jambo ambalo sijamkubalia.
“Nafikiri kutomkubalia kwangu dhahiri nahisi itakuwa ndicho kisa cha
kuamua kuondoka na kurudi nyumbani kwake, napata tabu sana na wimbo huu,
lakini naamini mimi ni mtu wa misimamao hivyo siwezi kuachana na
muziki kisa vitisho.
“Katika maisha hakuna jambo rahisi hasa kama wewe ni mpambanaji,
vitisho kama hivi sitaki kuvipatia nafasi ya kuniharibia maisha kwani
mimi ninachokifanya ni kuwakilisha mawazo ya wazalendo wengi ambao
imekuwa ni ngumu kila mmoja kufikisha maoni yake kwa jamii.
“Kuna watu wanadhani nilipoitwa na Mwakyembe nilienda kushikiwa akili
ili nibadili muziki wangu lakini ukweli ni kwamba, kule alikuwa akinipa
ushauri wa kawaida tu, hivyo hakuna jambo ambalo amenibadilisha
kwenye muziki wangu na nitaendelea kupigania ninachokiamini ili
nitimize ndoto yangu.
“Kifo kipo tu lakini wengi t u m e k u w a waoga wa kutangulia hasa
ukifikilia jamii inayokuzunguka, Wapo imenikutanisha na watu
nisiowafahamu, maana nakumbuka siku mbili nyuma zilizopita nilipigiwa
simu na mtu nisiyemjua akidai anahitaji kufanya biashara na mimi hivyo
nikaenda kuonana nae Ubungo.
“Huwezi kuamini ningekua muoga basi nisingemsikiliza maana baada ya
kukutana alinitoa chemba na kuanza kunihusia juu ya kuachana na wimbo
huo akidai watu wamejifanya kunichunia lakini hakuna anayefurahishwa,
hivyo kama nataka amani iendelee basi niuache na kingine akaniamia niwe
makini kwani kuna watu wana nia mbaya na mimi.
“Kusema kweli nimeshatishwa sana lakini watu wanachotakiwa kujua kama
kifo kipo basi nitakufa kwa kuwatetea mamilioni ya mashabiki zangu, ila
suala la kushikiwa akili au kubadilishwa gia yangu hapa halina nafasi,”
anasema Nay.
Ikumbukwe kwamba mwishoni mwa wiki iliyopita Nay baada ya kutoka Dodoma,
alikoenda kuitikia wito wa waziri Mwakyembe, alisema amefarijika kwa
namna moja au nyingine hasa baada ya kukutana, kwani walipata muda wa
kuketi na kuzungumza mambo mengi juu ya sanaa ya muziki.
Huku akimtaka kuwa makini na tunzi zake kwani zimekuwa na mfululizo wa
maneno ya kuwagusa watu moja kwa moja hivyo awe makini kwani kuna
wengine huwa si wavumilivu kwani asipojiahadhali wanaweza kuja kumdhuru
kwa namna moja au nyingine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni