Serikali imesema jumla ya walimu 3,081 wakiwemo walimu 7 wa shule ya
Sekondari Omumwani Kagera, wameajiriwa, hivyo bado kuna nafasi ya walimu
1.048 kati ya nafasi 4,129 za walimu wa Sayansi na Hisabati
zilizotolewa kibali cha ajira.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene alipokuwa
akizungumza na Waandishi Habari,ofsini kwake ambapo amewataka walimu
wote walioajiriwa wanatakiwa kuripoti katika vituo vyao vya kazi kuanzia
tarehe 18 hadi 25 mwezi huu.
Amesema walimu walioajiriwa wamepangwa moja kwa moja na TAMISEMI katika
halmashauri zote nchini ambazo zina upugufu wa walimu wa Sayansi na
Hisabati.
Simbachawene amesema kati ya walimu hao walioajairiwa walimu 1,537 ni wa Shahada na walimu 1,544 ni wa Stashahada.
“Sehemu kubwa ya walimu wa Shahada wamepangwa kwenye shule za kidato
cha tano na sita na wachache kwenye shule za kidato cha kwanza hadi cha
nne’’ alisema.
Simbachawene amekiri kuwa kuna upungufu wa walimu 26,026 wa masomo
Sayansi na Hisabati katika shule mbalimbali za sekondari nchini.
“Moja ya changamoto kubwa ambazo zinaikabili sekta ndogo ya elimu ya
sekondari ni upungufu wa walimu wa Sayansi na Hisabati upungufu uliopo
katika shule 3,602 ni 26,026 sawa na asilimia 60.14 ya walimu 43,248
wanaohitajika” amesema Simbachawene
Amesema walimu wanaohitajika kwa masomo hayo ni walimu 43,248 lakini waliopo kwa sasa ni 17,252 pekee.
Amesema kwa sasa serikali ina shule za sekondari 3,602 na kati ya hizo
shule 333 ni za kidato cha tano na sita huku zingine 54 za kidato cha
tano zimeanzishwa .
Aidha amesema shule hizo za sekondari kwa upande wa masomo ya Sanaa ina
ziada ya walimu 7,463 ambapo waliopo ni walimu 63,240 na wanaohitajika
ni walimu 55,777.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni