WAZIRI Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, amechambua
tofauti ya mazingira ya utawala wa awamu ya tatu, ambao ulikuwa na
changamoto ya kukosekana kwa fedha na kinachotokea sasa maarufu kusoma
namba.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Sumaye alisema
kuna tofauti nyingi lakini akaamua kuzungumzia kubwa zaidi kwa kujikita
katika mambo mawili; moja ni uchumi na lingine demokrasia na utawala
bora.
Sumaye ambaye ndiye Waziri Mkuu mwenye historia ya kukaa miaka kumi
mfululizo katika nafasi hiyo, alisema katika Awamu ya Tatu Serikali
iliimarishwa uchumi na kukuza na kuboresha nguzo kuu za uchumi, kwa
kujenga mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na kuingiza ushindani wa
kweli katika biashara.
Kwa mujibu wa Sumaye ambaye sasa ni kada wa Chadema, Awamu ya Tatu chini
ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa, ndiyo iliyojenga na kubuni vivutio
kwa wawekezaji wa ndani na wa nje na kuanzisha ushirikiano wa sekta ya
umma na binafsi (PPP) katika uwekezaji.
Sumaye aliendelea kueleza kuwa Awamu ya Tatu, ambayo hali yake ya
kukosena kwa fedha ilipewa jina la ‘Ukapa’ ndiyo iliyobuni na kuboresha
miundombinu ya uchumi kwa kuunda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na
Kituo cha Uwekezaji (TIC) pamoja na kuboresha sheria zilizoendana na
uchumi huria na wa kisasa.
Alisema hata maboresho ya miundombinu ya barabara, bandari na maji
yalianzia Awamu ya Tatu na katika huduma za jamii hasa elimu, awamu hiyo
ndiyo iliyobuni Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM),
uliopeleka watoto wote wenye umri wa kuanza shule darasani na Mpango wa
Maendeleo ya Elimu Sekondari (MMES).
“Awamu hii mengi ya mambo haya ni kinyume kabisa au hayatiliwi mkazo.
Kwa mfano Serikali imekwishatamka kuwa kuanzia mwaka huu wa fedha idara
za Serikali hazitapewa huduma na sekta binafsi. Hii ni kinyume kabisa na
sera ya PPP,” alisema.
Alisema hata sera ya utozaji kodi, inapaswa kujenga uhusiano mwema baina
ya mlipakodi na mtozakodi, lakini cha kushangaza hazishabihiani na
badala yake wafanyabiashara wengi wamefunga biashara zao.
Upatikanaji wa fedha
Akizungumzia hali ya upatikanaji fedha iliyopewa jina la ‘Ukapa’, Sumaye
alisema Awamu ya Tatu ilipoanza, hali ya uchumi ilikuwa duni na fedha
zilikuwa mikononi mwa wenye uchumi usio rasmi au uchumi wa magendo.
Alisema kazi ya kwanza ya Awamu Tatu, ilikuwa kurudisha uchumi katika
misingi sahihi na katika kufanya hivyo walikubaliana kuua biashara ya
magendo.
Alieleza kuwa kipindi hicho ndiyo watu wengi walipoona ugumu wa fedha
kupatikana wakauita 'Ukapa', lakini kipindi hicho hakikudumu muda mrefu,
kwani uchumi ulirudi katika misingi bora na kuimarika na watu wakaanza
kupata fedha kulingana na jasho lao halali.
Demokrasia
Sumaye alisema Awamu ya Tatu pia ilikuza demokrasia na utawala bora na
idadi ya vyama iliendelea kukua na vyama vya siasa vilifanya kazi za
kisiasa kwa uhuru bila kuzuiwa au kungiliwa.
Alifafanua kuwa utawala bora wakati wa Awamu ya Tatu, ulikuwa wa 'ukweli
na uwazi na uliofuata sheria’ na kutolea mfano wa nguzo tatu za dola
ambazo ni Utawala, Bunge na Mahakama kwamba zilifanya kazi kwa uhuru
bila nguzo moja kuingilia nyingine.
Waziri Mkuu huyo alisema watu walikuwa huru kutoa maoni yao bila
wasiwasi wala kamata kamata au watu kupotea bila maelezo yoyote kutoka
vyombo vya dola.
“Awamu hii ni kinyume kabisa na hivyo. Demokrasia imekandamizwa kiasi
kwamba vyama siasa havina uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara kama
sheria inavyotaka na uhuru wa vyombo vya habari umeminywa kabisa.
Mikutano ya Bunge haioneshwi tena mbashara katika luninga kama zamani,”
alisema.
Aliongeza kuwa hayo yote yanavunja Katiba ya nchi ibara ya 18 kwa sababu
ni haki ya kikatiba wananchi kuwa na uhuru wa kutoa, kupata au
kusambaza habari.
Alisema kwa sasa ni jambo la kawaida wapinzani kukumatwa bila sababu za
msingi na kukaa rumande muda mrefu kuliko saa 48 zinazoruhusiwa kisheria
na hata wengine kufungwa jela.
Kwa mujibu wa Sumaye, hata kupotea kwa watu wenye mawazo tofauti na
Serikali au 'kuvamiwa na watu wasiojulikana' kumeanza kuwa jambo la
kawaida.
Credit - Jambo leo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni